Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ametaka kuchukuliwa kwa hatua za haraka kutengeneza upya miundombinu nchini, hasa reli na barabara, iliyoharibiwa kutokana na mvua na mafuriko ya wiki za karibuni katika baadhi ya mikoa nchini.Mheshimiwa Rais pia amehimiza ushirikiano wa karibu kati ya taasisi za kiraia na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika kukabiliana na kazi ya kukarabati miundombinu hiyo.“Uchumi huu utaishiwa sana nguvu kama hatukushughulikia haraka suala la kukarabati miundombuni na hasa reli,” Rais Kikwete amekiambia kikao cha dharura alichokiitisha mchana wa leo, Jumatatu, Januari 25, 2010, Ikulu, Dar es Salaam, kujadili kiwango cha uharibifu na jinsi ya kunusuru miundombinu ya reli na barabara.Rais Kikwete aliagiza kufanyika kwa kikao hicho Ijumaa iliyopita, Januari 22, 2010, wakati alipoendesha kikao cha Baraza la Mawaziri.Waziri wa Miundombinu, Mheshimiwa Dkt. Shukuru Kawambwa amewaongoza maofisa waandamizi kutoka wizara yake na kutoka baadhi ya makampuni na mashirika yaliyoko chini ya wizara yake, ikiwamo Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) na Wakala wa Barabara (Tanroads) katika kikao cha leo.Katika kikao hicho, maofisa hao walimweleza Rais Kikwete uharibifu uliofanyika katika Reli ya Kati na hasa kati ya Stesheni za Gulwe na Kilosa, katika mikoa ya Dodoma na Morogoro, kutokana na mvua zilizonyesha katika wilaya za Mpwapwa na Kilosa kati ya Desemba 24, mwaka jana, 2009 na Januari 10, mwaka huu, 2010.Katika maeneo ya Kilosa, mvua hizo na mafuriko yaliyoandamana na mvua hizo, yameng’oa kabisa sehemu ya Reli ya Kati na kusimamisha huduma za reli hiyo kati ya Dar es Salaam na Dodoma.Sababu kubwa za uharibifu huo ni kufurika na kwa mito ya Mkondoa na Kinyasungwi, hali iliyosababisha kuhama kwa mito hiyo kutoka katika njia za asili na kuelekea kwenye tuta la reli.Maofisa hao wamemweleza Rais Kikwete kuwa zipo sehemu 28 zilizoharibika kati ya stesheni hizo mbili lakini ni sehemu 26 zilizoaharibika zaidi. Pia wamemweleza kuwa madaraja tisa yamesombwa na maji na mengine matatu yako katika hatari ya kusombwa.Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu, Mhandisi Omar Chambo pia amemweleza Rais Kikwete mipango ya ukarabati wa sehemu hiyo ya reli na kuahidi kuwa kazi hiyo inaweza kuwa imekamilika kati ya miezi miwili na miezi mitatu.Kuhusu uharibifu kwenye barabara, Mhandisi Chambo amesema kuwa uharibufu kwenye barabara umefanyika katika mikoa 18 ya Tanzania Bara.Mikoa hiyo ni Arusha, Dodoma, Iringa, Kagera, Kilimanjaro, Kigoma, Lindi, Manyara, Mara, Mbeya, Morogoro, Mtwara, Mwanza, Rukwa, Shinyanga, Singida, Tabora na Tanga.Mhandisi Chambo amesema kuwa kiasi cha sh bilioni 13.286 zinahitajika kuweza kukarabati barabara hizo ambazo zimeharibika kwa viwango tofauti huku uharibifu mkubwa ukiwa umetokea katika Mkoa wa Dodoma ambako barabara zake tatu hazipitiki.Imetolewa na:Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,Ikulu,DAR ES SALAAM.25 Januari, 2010
MSD YAPONGEZWA KWA MABORESHO YA HUDUMA MKOANI KAGERA
-
Bohari ya Dawa (MSD) imepongezwa kwa kuimarisha mnyororo wa ugavi wa bidhaa
za afya mkoani Kagera, ambao umepunguza malalamiko ya upungufu wa bidhaa za
a...
48 minutes ago