Ukimuona ni paka wa kawaida ambaye hana tofauti yoyote na paka wengine lakini inasemwa kuwa ana uwezo wa kuwatambua wagonjwa wanaokaribia kufariki hospitalini na hadi sasa imesemwa kuwa ameishafanikiwa kuvinusa vifo vya wagonjwa 50 kabla hata havijatokea
Paka anayejulikana kwa jina la Oscar hujisogeza na kukaa karibu na kitanda cha mgonjwa aliyebakiza muda mchache kufariki.Iwapo ndugu wa mgonjwa huyo watamfukuza paka huyo nje ya chumba cha mgonjwa wao na kumfungia mlango, basi paka huyo hugoma kuondoka na huanza kuukwaruza mlango kwa nguvu aking'ang'ania kuingia ndani.Paka Oscar ambaye huishi katika nyumba moja ya kutunza wagonjwa wazee iliyopo kwenye mji wa Province katika jimbo la Rhode Island nchini Marekani hupenda kuzungukazunguka toka chumba kimoja hadi kingine katika nyumba hiyo.Inadaiwa kuwa Paka Oscar huwa hapendi kutumia muda wake pamoja na vikongwe katika nyumba hiyo isipokuwa wale tu ambao wanakaribia kufariki.Tabia ya paka huyo ambaye hivi sasa ana umri wa miaka mitano, iligunduliwa mwaka 2007 na manesi wa nyumba hiyo ambao kwa jinsi walivyo na uhakika na uwezo wa paka Oscar huwataarifu familia ya mgonjwa anayezungukiwa sana na paka huyo kuwa mambo yanaelekea kuwa mabaya.Katika kuonyesha uwezo wa paka huyo, siku moja manesi walimchukua paka huyo na kumweka kwenye kitanda cha mgonjwa ambaye waliamini atafariki dakika yoyote ile, lakini paka huyo alichoropoka na kukimbilia chumba cha pili yake.Uamuzi wa paka Oscar ulijionyesha siku hiyo hiyo kwa mgonjwa wa chumba cha pili kufariki siku hiyo hiyo jioni wakati mgonjwa wa chumba cha kwanza aliendelea kuishi kwa angalau siku mbili kabla ya kufariki paka Oscar akiwa amerudi pembeni ya kitanda chake.Wataalamu hivi sasa wanamfanyia uchunguzi paka huyo ambaye alianza kulelewa kwenye hospitali hiyo tangia alipokuwa kichanga.Mmmoja wa wanasayansi anayemfanyia uchunguzi paka huyo, Dr David Dosa, ameelezea mshangao wake kwa uwezo wa paka huyo kutabiri bila kukosea vifo vya wagonjwa 50 katika kipindi cha miaka mitano.Dokta Dosa anasema kuwa hakuna maelezo yoyote ya kisayansi kuelezea tabia ya paka huyo.Katika tukio jingine, mwanaume mmoja aliyetajwa kwa jina la Richards aliamua kukaa pembeni ya kitanda cha mama yake muda wote baada ya madaktari kumwambia kuwa mama yake aliyekuwa mgonjwa mahututi angefariki muda wowote ule.Richard bila kupumzika alikaa pembeni ya kitanda cha mama yake kwa siku tatu mfululizo lakini mama yake hakufariki.Madaktari walimshauri Richard aende nyumbani kwake akapumzike kidogo kabla ya kurudi baadae. Richard kwa shingo upande alikubali kuondoka kwenda kwake kupumzika.Muda mfupi baada ya kuondoka, mama yake alifariki. Hakufariki akiwa peke yake bali Oscar alikuwa pembeni yake.