Ndege ya Yemen yaanguka Comoro
Ndege ya abiria ya Yemeni ikiwa na watu zaidi ya 150 imeanguka katika bahari ya Hindi karibu na visiwa vya Comoro.
Baadhi ya miili imepatikana na waliosalimika kuokolewa, maafisa kutoka shirika la ndege hiyo, Yemenia, wameeleza.
Ndege hiyo muundo wa Airbus 310 ikiwa na safari namba IY626 ilikuwa ikisafiri kutoka Sanaa mji mkuu wa Yemen, lakini idadi kubwa ya abiria walianzia safari yao Ufaransa.
Chanzo cha ajali hiyo bado hakijajulikana. Waziri mmoja wa Ufaransa amesema hitilafu kadhaa ziligundulika wakati ndege hiyo ilipokaguliwa maswala ya kiufundi mwaka 2007.
"Ndege aina ya A310 iliyohusika ilikaguliwa mwaka 2007 na mamlaka ya usafiri ya Ufaransa (DGAC) na waligundua hitilafu kadhaa. Tangu wakati huo ndege haijawahi kurejea Ufaransa," Waziri wa Usafirishaji wa Ufaransa, Dominique Bussereau alinukuliwa akiieleza televisheni moja ya Ufaransa.
"Kampuni hiyo haikuwa katika orodha ya makampuni yaliyopigwa marufuku lakini ilikuwa chini ya uangalizi wa masharti magumu ya ukaguzi, na ilikuwa ikitarajiwa kuhojiwa na kamati ya maswala ya usalama ya Umoja wa Ulaya."
Awali Bw Bussereau alivieleza vyombo vya habari vya Ufaransa kuwa hali mbaya ya hewa huenda ilisababisha ajali hiyo.
Ramani inayoonyesha njia ilikopita ndege hiyo.
Taarifa zinaeleza kuwa ndege hiyo ilikuwa ikitarajiwa kutua Moroni mji mkuu wa Comoro majira ya saa nane na nusu. Abiria wengi kati yao walisafiri kwenda Sanaa wakitokea Paris na Marseille kwa kutumia ndege tofauti.
Ndege hiyo waliyounganisha kwenda Moroni inasemekana ilisimama kwa muda nchini Djibouti.
Kulikuwa na watu zaidi ya 150 ndani yake wakiwemo watoto wachanga watatu na wafanyakazi 11.Habari katika picha