MCHEZA mieleka maarufu duniani, Eki “Eddie” Fatu ambaye anajulikana kwa jina la “Umaga” amefariki Ijumaa iliyopita huko Houston, Marekani, kutokana na shambulio la moyo.Kifo cha mwanamichezo huyo, kimeongeza orodha ya wacheza mieleka wa kulipwa ambao wamefariki wakiwa hawajafikia umri wa miaka 40.
Fatu, aliyekuwa na umri wa miaka 36, na ambaye alipata umaarufu mkubwa hivi karibuni katika medani ya mieleka chini ya chama cha World Wrestling Entertainment (WWE) akitumia jina la “Umaga,” alikutwa na mkewe akiwa amezimia katika chumba chake huko Spring, Texas, na hivyo akamkimbiza hospitali.
Umaga alipatwa na shambulio jingine la pili la moyo akiwa hospitalini hapo na akafariki.
Fatu, mtu ambaye alikuwa anafahamika kutokana na michoro (tattoo) iliyokuwa usoni mwake, anatoka katika familia kubwa ya wapigana mieleka wa Samoa ambao wameifanya biashara ya mchezo huo kuwa maarufu kwa vizazi kadhaa.
Umaarufu wao ulianzia kwa baba zake wadogo, Afa na Sika Anoi’a, ambao walijulikana katika medani hiyo kama “Wasamoa wa Msituni” (The Wild Samoans) mnamo miaka ya 1970 na 1980.
Mtu maarufu zaidi katika ukoo huo alikuwa ni binamu yake aliyeitwa Dwayne “The Rock” Johnson, ambaye aliacha mieleka na kujikita katika medani ya filamu huko Hollywood.
Kilele cha mafanikio ya Fatu kilikuwa mwaka 2007 aliposhiriki tamasha la Wrestlemania 23 huko Detroit ambalo liliwapa umaarufu mkubwa, mmiliki wa WWE, Vince McMahon na Donald Trump.
Hata hivyo, umaarufu wake ulikuwa wa muda mfupi na aliondolewa katika mkataba wa WWE tarehe 8 Juni alipokataa kwenda katika kituo cha huduma ya kuachana na matumizi ya madawa ya kulevya, baada ya kwenda kinyume na sera ya matumizi ya madawa hayo kwa mujibu wa WWE.
Ni hivi karibuni tu alikuwa amerejea katika ziara binafsi ya maonyesho ya mieleka aliyoifanya Australia ambapo alikumbwa na tatizo hilo ambalo liliondoa uhai wake.
“Kwa niaba ya familia yangu, familia ya Anoa’i na Fatu, tumesikitishwa na kushitushwa na kifo cha Eki wetu,” Afa Anoa’i aliliambia gazeti la Wrestling Obeserver.
“Kwetu alikuwa ni mtoto, binamu, kaka, mume, na baba yetu. Mioyo yetu imekumbwa na simanzi na hakuna maneno yanayoweza kuelezea hisia zetu. Ni jambo la faraja kufahamu Eki alivyopendwa na familia yake, watu wa rika lake, marafiki na wapenzi wake wote.”
Idadi kubwa ya wacheza mieleka vijana wamekufa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, na kuwafanya baadhi yao kuamini kwamba mchezo huo una laana.
Miongoni mwa matukio mabaya zaidi yalimhusisha Chris Benoit (40) ambaye alijiua huko Georgia mwaka 2007 baada ya kumwua mkwe, Nancy, na mwanaye Daniel.
Mwingine ni Eddie Guerrero (38) aliyekufa kwa shambulio la moyo mwaka 2005 huko Minnesota katika hoteli moja.
Mcheza mieleka Owen Hart (33) naye alikufa huko Kansas City mwaka 1999 baada ya kuumia katika onyesho lililokuwa likichukuliwa na televisheni.
Vilevile, mnamo Machi mwaka huu, mcheza mieleka mwingine wa zamani wa WWE, Andrew “Test” Martin (34), alifariki kwa kutumia kiwango kikubwa zaidi cha madawa ya Oxycontin.